Silabi na vitanzandimi vya sauti d na nd
- Je, unayajua maneno gani yenye silabi za sauti d na nd? Mtajie mwenzako.
- Mkiwa katika vikundi kama mtakavyoelekezwa na mwalimu wenu, undeni na mzitamke silabi za sauti d na nd. Fuateni mfano ufuatao:
sauti ya konsonanti | d | d | d | d | d |
sauti za vokali | a | e | i | o | u |
silabi za sauti d | da | de | di | do | du |
- Sikilizeni silabi za sauti d na nd zikitamkwa na mwalimu wenu.
- Sikilizeni maneno yafuatayo yaliyo na silabi za sauti d na nd yakitamkwa na mwalimu wenu:
- dada, ndani
- debe, ndevu
- dirisha, ndimu
- dobi, ndoto
- dunia, nduru
- duka, ndugu.
- Tamkeni majina ya picha zifuatazo:
- Tambueni na mzitamke silabi za sauti d na nd katika majina mliyoyatamka katika Shughuli ya 5.
- Mkiwa wawiliwawili, tamkianeni maneno mengine yenye silabi za sauti d na nd mnayoyajua.
- Je, unavijua vitanzandimi vyovyote vyenye silabi za sauti d na nd? Wakaririe wenzako vitanzandimi hivyo.
- Sikilizeni vitanzandimi hivi vikikaririwa na mwalimu wenu.
- Fundi stadi ameliunda dawati maridadi na kuliingiza ndani ya darasa.
- Dada Rukia amenunua: dafu, andazi, degi, tende, dishi, ndizi, dodoki, ndoo, dugu na ndusi.
- Dobi aliibeba ndoo na dodoki kisha akaondoka na kwenda madobini.
- Dada Farida hakulidandia daladala kwa kuwa daima kulidandia daladala ni hatari.
- Aliokota maembedodo yaliyodondoka na kuyaweka katika ndoo ndogo iliyokuwamo ndani ya gari dogo.
- Tambueni na mzitamke silabi za sauti d na nd katika vitanzandimi mlivyovisikiliza katika Shughuli ya 9.
- Karirianeni vitanzandimi vya Shughuli ya 9.
- Undeni vitanzandimi vyenye silabi za sauti d na nd.
- Karirini vitanzandimi mlivyoviunda katika Shughuli ya 12 mbele ya wenzenu ili wavitolee maoni na waviboreshe.
- Katika wakati wako wa ziada, unda vitanzandimi vyenye silabi za sauti d na nd. Viandike vitanzandimi hivyo kwenye tarakilishi au daftarini.
- Watumie wenzako kwa baruapepe au uwape daftari lenye vitanzandimi ulivyoviunda katika Shughuli ya 14 ili waviboreshe na kuvikariri.
Silabi na vitanzandimi vya sauti ch na sh
- Je, unayajua maneno gani yenye silabi za sauti ch na sh? Mtajie mwenzako maneno hayo.
- Mkiwa katika vikundi kama mtakavyoelekezwa na mwalimu wenu, undeni na mzitamke silabi za sauti ch na sh. Fuateni mfano ufuatao:
sauti ya konsonanti | ch | ch | ch | ch | ch |
sauti za vokali | a | e | i | o | u |
silabi za sauti ch | cha | che | chi | cho | chu |
- Sikilizeni silabi za sauti ch na sh zikitamkwa na mwalimu wenu.
- Sikilizeni maneno haya yaliyo na silabi za sauti ch na sh yakitamkwa na mwalimu wenu:
- chaki, shaki
- cheka, sherehe
- chimba, shiba
- chora, shona
- chuo, shupavu
- chuma, shume.
- Tambueni na mzitamke silabi za sauti ch na sh katika maneno mliyoyasikiliza katika Shughuli ya 4.
- Tamkeni majina ya picha zifuatazo:
- Tambueni na mzitamke silabi za sauti ch na sh katika majina mliyoyatamka katika Shughuli ya 6.
- Mkiwa wawiliwawili, tamkianeni maneno mengine yenye sauti ch na sh mnayoyajua.
- Je, unavijua vitanzandimi vyovyote vyenye silabi za sauti ch na sh? Wakaririe wenzako vitanzandimi hivyo.
- Sikilizeni vitanzandimi hivi vikikaririwa na mwalimu wenu.
- Alishuka akalichukua shuka lenye picha ya shoka kabla ya sherehe ili lisichezewe na kuwa chafu.
- Wanachama wa chama cha shirika la mashamba wameyachimba mashimo katika sehemu chache za mashamba yao.
- Wapishi wachache wacheshi shereheni wamekamilisha kukitayarisha chakula chema na cha kutosha.
- Usimwache mtoto mchanga awashe cheche za moto zinazoweza kuchacha na kusababisha maafa.
- Mshonaviatu hakuchoka kushiriki kuyachimba mashimo ya kutupia taka ili zisichomwe na kusababisha moshi unaoyachafua mazingira.
- Tambueni na mzitamke silabi za sauti ch na sh katika vitanzandimi mlivyovisikiliza katika Shughuli ya 10.
- Karirianeni vitanzandimi katika Shughuli ya 10.
- Undeni vitanzandimi vyenye silabi za sauti ch na sh.
- Karirini vitanzandimi mlivyoviunda katika Shughuli ya 13 mbele ya wenzenu ili wavitolee maoni na kuviboresha.
- Katika wakati wako wa ziada, unda vitanzandimi vyenye silabi za sauti ch na sh. Viandike vitanzandimi hivyo kwenye tarakilishi au daftarini.
- Watumie wenzako kwa baruapepe au uwape daftari lenye vitanzandimi ulivyoviunda katika Shughuli ya 15 ili waviboreshe na kuvikariri.