Mahojiano
Kichocheo
- Tazama picha hii.
- Mweleze mwenzako ni nini kinachoendelea katika picha uliyotazama.
- Kwa nini ni muhimu kusikiliza kwa makini unapohojiwa? Waeleze wenzako darasani.
- Ni mambo gani unayopaswa kufanya ili uweze kupata ujumbe vizuri wakati wa mahojiano?
Shughuli ya 1
Ukiwa katika kikundi:
- Tazama mahojiano ya mwalimu na mwanafunzi darasani au yaliyorekodiwa katika video.
- Waeleze wenzako vitendo ambavyo mhojiwa alifanya kuonyesha kuwa alisikiliza mahojiano. Maswali yafuatayo yatakuelekeza:
- Ni nini kinachoonyesha kuwa alisikiliza kwa makini?
- Alimtazama mzungumzaji vipi?
- Je, alitumia viziada lugha gani?
Shughuli ya 2
Mkiwa wawiliwawili:
- Tazameni tena mahojiano ya mwalimu na mwanafunzi au yale yaliyorekodiwa katika video.
- Tambueni vipengele vya kusikiliza na kujibu mahojiano ambavyo mhojiwa alizingatia wakati wa kujibu mahojiano. Tumia maswali yafuatayo kukuelekeza:
- Ni nini kinachoonyesha kuwa alitumia lugha ya adabu?
- Ni mambo gani yanayoonyesha kuwa alizungumza kwa ukakamavu?
- Je, ni mambo gani yanayoonyesha kuwa mhojiwa alikuwa anasubiri hadi mzungumzaji amalize kuzungumza?
- Ni nini kinachoonyesha kuwa mhojiwa alitaka ufafanuzi zaidi?
- Ni nini kinachoonyesha kuwa mhojiwa alijibu wakati ufaao?
Shughuli ya 3
- Mkiwa wawiliwawili, igizeni mahojiano kati ya chifu na mwanakijiji kuhusu usafi wa soko lenu. Zingatieni:
- kusikiliza kwa makini,
- kuepuka vizuizi vya mawasiliano kama vile kelele, matamshi, yanayotatanisha na sauti hafifu,
- kumtazama mzungumzaji ana kwa ana,
- kutumia viziada lugha kuonyesha kulielewa swali au wazo,
- kudadisi au kuomba ufafanuzi,
- kutumia lugha ya adabu,
- kuzungumza kwa ukakamavu,
- kutomkata kalima mzungumzaji,
- kujibu wakati ufaao.
- Nakili daftarini jedwali lifuatalo. Tathminianeni kuonyesha ikiwa kila mmoja wenu alizingatia vipengele vilivyotajwa katika kusikiliza na kujibu mahojiano.
Orodha ya ukaguzi
Jina la mwanafunzi:
Kutumia vipengele vya kusikiliza mahojiano. | Kutumia vipengele vya kujibu mahojiano. | |||
Ndiyo | La | Ndiyo | La | |
Alisikiliza kwa makini. | ||||
Alimtazama mzungumzaji. | ||||
Alidadisi. | ||||
Alitumia lugha ya adabu. | ||||
Alizungumza kwa ukakamavu. | ||||
Alijibu wakati ufaao. |
Maoni ya mwalimu:
Tarehe:
- Mpe mwalimu ili akupe maoni yake kuhusu jedwali lililotumika kukutathmini.
Wazo bainifu
Nimegundua kuwa:
- Ninaposikiliza mahojiano ninafaa kusikiliza kwa makini, kuepuka vizuizi vya mawasiliano, kumtazama mzungumzaji ana kwa ana na kutumia viziada lugha.
- Ninapojibu mahojiano ninafaa kutumia lugha ya adabu, kuzungumza kwa ukakamavu, kutomkata kalima mzungumzaji, kudadisi na kujibu wakati ufaao.
Changamkia
Mkiwa darasani, fanyeni mahojiano na kiranja. Muulizeni kuhusu usafi wa vyoo vya shule. Tumieni maswali yafuatayo:
Hojaji kuhusu usafi wa vyoo shuleni.
- Shule hii ina vyoo vingapi?
- Vyoo vya shule husafishwa mara ngapi kwa siku?
- Vyoo vya shule husafishwa na nani?
- Je, wanaosafisha vyoo hutumia nini kusafisha?
- Ungependa wanafunzi waambiwe nini kuhusu kudumisha usafi wa vyoo shuleni?
Shirikisha mzazi au mlezi
- Ukiwa nyumbani, sikiliza mahojiano katika kifaa cha kidijitali kama vile redio au televisheni.
- Mweleze mzazi au mlezi kuhusu jinsi vipengele vya kusikiliza na kujibu mahojiano vilivyozingatiwa katika mahojiano ya swali la 1.